Wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitengua
uamuzi wake wa kung’atuka kwenye wadhifa huo na kuomba kurejea, viongozi
wa juu wa chama hicho wamepinga hatua hiyo wakisema katiba yao
hairuhusu na kwamba anakwenda kukiua chama.
Kauli za viongozi hao, zimekuja muda mfupi baada ya Profesa Lipumba
kutangaza nia hiyo jana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho,
Buguruni huku akibainisha kuwa amefanya hivyo baada ya kuombwa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba
hawezi kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa
kwenye nafasi aliyoikataa.
“Anataka kuja kukiharibu chama,” alisema Mazrui. Alifafanua kuwa tayari
chama hicho kimefanya mambo mengi bila Lipumba ambaye alikuwa anaona
kila kinachoendelea, hivyo alichokisema hakina mashiko kwani CUF
ilisharidhia kuitisha mkutano wa uchaguzi kujaza hiyo.
Akieleza sababu alizozitoa mwenyekiti huyo, Mazrui alisema haoni
chochote cha maana. “Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni
nini?” alihoji naibu katibu mkuu huyo.
Alisisitiza kuwa Wazanzibari wanaendelea na mchakato wa kuidai haki yao
iliyoporwa Oktoba 25 na hawana nafasi ya kushughulika na masuala
yasiyokuwa na tija kwao, hivyo haoni kama kuna sababu ya kumjadili
Lipumba na nafasi yake badala ya kuendelea pale walipo.
“CCM wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja
kuharibu mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili.Tunataka haki
iliyoporwa,” alisisitiza.
Msimamo wa Mazrui haukutofautiana sana na ule wa Kaimu Mwenyekiti wa
chama hicho, Twaha Taslima aliyebainisha kuwa amesikia taarifa za kurudi
kwa Profesa Lipumba, lakini haoni uwezekano huo.
“Katiba hairuhusu hilo.Hakuna kifungu kinachotoa nafasi kwa kiongozi
aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake pindi atakapotaka kufanya hivyo,”
alisema Taslima.
Aliielezea Ibara ya 117 (2) iliyotumiwa na Profesa huyo kuandika barua
ya kutengua uamuzi wake, kuwa inatoa tafsiri zaidi ya moja hivyo kuwapo
haja ya viongozi kukutana na kujadili suala hilo kabla ya kutoa maamuzi.
Kwa kuwa hakuwapo kwenye mkutano huo, Taslima alisema: “Tunahitaji
kukutana haraka na kujadili. Tutafanya mkutano wetu na tutavijulisha
vyombo vya habari ndani ya wiki hii.”
Taslima alisema kipindi alichoongoza kilikuwa na changamoto nyingi
ambazo ni tofauti na sasa, hivyo haoni haja ya mtu mwingine kuja wakati
mambo yametulia. Chama hicho kilipanga kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi
hiyo Agosti mwaka huu.
Baada ya kung’atuka kwa Lipumba, Taslima alichukua mikoba yake na
kukivusha chama hicho kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana,
pamoja na ule wa Zanzibar ambao uliahirishwa na chama hicho kususia
marudio yake Machi 20 mwaka huu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya
alisema upo uwezekano wa Lipumba kurudi kwenye nafasi yake kwasababu
mpaka sasa haijazibwa.
“Mwenyekiti huchaguliwa au kutenguliwa na halmashauri kuu. Haikupitisha
kujizulu. Barua ya kujiuzulu itaenda pamoja na hii ya kutengua uamuzi wa
awali,” alisema Kambaya.
Kauli ya Lipumba
Awali, Profesa Lipumba alisema mara kadhaa amekutana na viongozi wa dini
na chama pamoja na wanachama wa CUF na wote walikuwa na ujumbe mmoja
tu…’rudi tukijenge chama.’
Profesa Lipumba hakushiriki mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,
mwaka jana ambao kwa upande wa Zanzibar, kutokana na hitilafu
zilizojitokeza ulifutwa na kurejewa Machi 20 mwaka huu huku chama hicho
kikiwa kimesusia marudio hayo.
Pamoja na hayo yote, Lipumba alisema ametafakari sana juu ya hali ya
kisiasa Zanzibar na kuona umuhimu wa kutoa ushirikiano ili mambo yaende
kwa manufaa ya taifa.
“Ni lazima nchi iendeshwe kwa misingi ya demokrasia ambayo itapatikana
kwa umoja wetu.Nimerudi kushirikiana na wenzangu kutimiza malengo hayo
ili kuchangia maendeleo ya Tanzania,” alisema Profesa Lipumba.
Lipumba aliachana na uongozi wa chama hicho, Agosti 8, mwaka jana, siku
chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kukubaliana kumsimamisha Edward
Lowassa.
Alimuandikia barua Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa
hakubaliani na uamuzi wa chama chake kuridhia makada waliohama Chama cha
Mapinduzi (CCM), akiwemo Lowassa, kupewa fursa ya kugombea nafasi za
uongozi.
Baada ya kukatwa kwenye mchujo wa ndani ya CCM, Lowassa akiwa na makada
kadhaa wa chama hicho akiwamo aliyewahi kuwa waziri mkuu, Frederick
Sumaye, alihamia Chadema ambako alipewa fursa ya kupeperusha bendera ya
chama hicho kilichomo ndani ya Ukawa.
Lipumba hakukubaliana na hilo, alikaa pembeni na kuachia ngazi ingawa alishiriki tukio la kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa.
Jana, wakati anatangaza kufanya mabadiliko ya kile alichokiamua miezi 10
iliyopita, hakuruhusu maswali, ila alifafanua kile kitakachofuata baada
ya kuwasilisha ombi hilo, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho: “Katibu
Mkuu anashauriana na wanasheria kabla suala langu halijapelekwa kwenye
halmashauri kuu kama katiba inavyosema,” alisema Profesa Lipumba.
Post a Comment