KUFUNGIWA NA KUPIGWA MARUFUKU KWA WIMBO WA ‘PALE KATI PATAMU’ WA MSANII EMMANUEL ELIBARIKI ‘AKA’ NEY WA MITEGO
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati
patamu’ ulioimbwa na Msanii Ney wa Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa
wa maadili.
Msanii huyu amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa
yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka
maadili. Kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke
sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada
mbalimbali.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA
namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda
maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi
yoyote ya sanaa.
ikumbukwe kwamba BASATA limeshamuita na kumuonya msanii huyu mara kadhaa
kutokana na tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi
kubadilika na kuachana na tabia hiyo. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya
matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa
maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye
kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. Kwa sasa
Msanii huyu ametoa wimbo mwingine wa Pale Kati patamu ambao uko
mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu
yaani uchi wa mnyama.

No comments:
Post a Comment